Wednesday, May 11, 2011

Wanafunzi Serya Sekondari wayakimbia mabweni




Image
Dada Mkuu wa Shule ya Sekondari Serya, Leila Rashid, akionesha sehemu ya vitanda ambavyo viko wazi kwa kukosa wanafunzi.




UJENZI wa mabweni katika shule za sekondari za kata nchini umekuwa ukipigiwa kelele na baadhi ya wananchi na hata wanafunzi wenyewe.

Hali hiyo inatokana na baadhi ya shule kujengwa mbali na makazi ya watu, hali inayosababisha wanafunzi wengi kutembea umbali mrefu. Umbali huo unawasababisha
wanafunzi wanapofika shuleni, kuwa wamechoka na pindi walimu wanapoingia darasani, wanatumia nguvu kubwa kufundisha huku wanafunzi wakiwa hawapokei.

Suala la umbali linalalamikiwa kuwa chanzo cha wanafunzi wanaomaliza kidato cha nne wa shule hizo, kufanya vibaya kutokana na wanafunzi wengine kutoka mazingira duni yasiyokuwa na taa na yasiyokuwa rafiki, kwa kumsaidia kusoma zaidi.

Licha ya kwamba mabweni yamekuwa ni tatizo, katika shule hizo ipo shule nyingine ambayo wanafunzi wake wameyakimbia mabweni na kusababisha vitanda kubaki wazi.

Hali hiyo imejidhihirisha wazi katika Shule ya Sekondari ya Serya iliyoko katika Kata ya Sururu, wilayani Kondoa mkoani Dodoma umbali wa kilomita 20 kutoka Kondoa mjini ambapo wanafunzi wake wa kike wamekwepa kukaa katika mabweni kutokana na madai kuwa wazazi wao wamekosa mwamko wa elimu.

Akizungumzia hali ya shule hiyo hivi karibuni, Mkuu wa shule hiyo, Festo Kangalawe, anasema kama kuna kitu kinachomhuzunisha ni jinsi ambavyo ufaulu wa wanafunzi wa kike katika shule hiyo, umekuwa ni wa kiwango cha chini na kwamba anajitahidi, lakini bado hajayaona mafanikio.

Anasema shule hiyo ilianzishwa mwaka 2007. Katika matokeo ya kidato cha nne mwaka jana, wanafunzi 33 walipata daraja la nne na wanafunzi 41 walipata daraja sifuri. Kuhusu mabweni, anasema shule ilipata bahati ya kupata mfadhili, ambaye aliweka mtambo unaotoa umeme kutokana na mwanga wa jua (solar) katika darasa shuleni hapo.

Lengo lilikuwa ni kuwasaidia wanafunzi wanaolala mabwenini kujisomea usiku. Anasema bweni moja lililojengwa shuleni hapo lina vitanda 48, ambapo uongozi ulitoa kipaumbele kwa wanafunzi wa kike kuishi bure katika mabweni hayo ili waweze kujisomea zaidi na kuongeza kiwango cha ufaulu.

Jambo la kushangaza ni kwamba licha ya kutoa kipaumbele kwa wanafunzi hao wa kike, ni wanafunzi 22 ndio walioingia, huku wengine wakiendelea kurudi majumbani kwao na kuacha vitanda vikiwa wazi.

Hali hiyo inatokana na wazazi wao, kudai kuwa watoto wao wana kazi nyingi za kufanya, ikiwa ni pamoja na kwenda kutafuta maji, kuchunga ng’ombe na wakati mwingine kuwatuma dukani.
Aidha, anashukuru vyombo vya habari kuwafikia, na kwamba hii ni mara ya kwanza kuwafikia tangu shule hiyo ilipoanzishwa.

Wanafunzi wengi wanaosoma shuleni hapo, wanatoka vijiji vya mbali, hali inayosababisha wakati wa mvua kutokufika shuleni kutokana na mito kufurika maji, hivyo kushindwa kuvuka.
Hali hiyo ndiyo iliyosababisha uongozi kutoa kipaumbele kwa wasichana kukaa katika mabweni hayo ili kuinua zaidi uwezo wao kielimu.

Akizungumzia matokeo ya mtihani wa kidato cha nne kwa mwaka jana, anasema yamewasikitisha, haswa ikizingatiwa kuwa walikodi hata walimu wa mtaani ili shule hiyo iweze kuonekana katika ramani ya dunia, kwa kufaulisha kwa kiwango kikubwa.

Pia, serikali ilipofuta mtihani wa kidato cha pili mwaka 2008 ilisababisha matokeo kuwa mabaya zaidi kwani wanafunzi hawakuwa na mwamko wa kujisomea kwa kuwa walijua wazi hakuna mtihani wa mchujo.

Kadhalika anasema katika kuangalia ufaulu wa kidato cha nne, ni vyema kuangalia pia ngazi ya elimu ya msingi, walimu wake wanafundisha ipasavyo, na vilevile vitabu na miundombinu kwa wanafunzi ni ya kuwasaidia kusoma kwa bidii.

Kuhusu walimu, anasema shule ina walimu watatu, ambao wanafundisha idadi ya wanafunzi 134 na kiwango cha walimu ni diploma. Walimu wa sayansi ni tatizo kubwa. Shule hiyo haina walimu wa fizikia na baiolojia.

Kwa masomo ya kemia na hisabati, yupo mmoja anayefundisha shule nzima. Kadhalika , yupo mwalimu mmoja wa kidato cha sita anayefundisha masomo ya baiolojia na jiografia.

Kwa upande wa maabara, anasema wanafunzi wake hawavijui vifaa vya kufanyia mazoezi, kama vile test tube, ambapo wamekuwa wakiviona katika michoro na picha tu, kwa kuwa shule hiyo haijabahatika kuwa na kifaa chochote.

Anasema wanafundisha katika mazingira magumu, na kwamba inapofikia wakati wa mtihani, wanafunzi hufanya mtihani wa nadharia pekee yake ; na sio wa vitendo. Kadhalika, walimu wote wanaofundisha hapo, wanatoka nje ya shule hiyo umbali wa kilomita tatu hadi nne,
kutokana na kukosa nyumba za kuishi shuleni hapo.

Wamekuwa wakiishi katika nyumba moja huko uraiani, kwa kugawana chumba kimojakimoja.
Kuhusu mtihani wa kidato cha pili, walimu hao walitaka serikali iurejeshe. Walisema kukosekana kwa mtihani huo, kumepunguza wimbi la wanafunzi kujituma.

Walitaka pia kiwango cha ufundishaji kwa shule ya msingi, kitazamwe upya. Anasema shule hiyo, haina maji, ambapo wanafunzi hulazimika kufuata maji kilomita nne tena katika korongo
na kurejea kuendelea na masomo.

Kuhusu hali ya vitabu, anasema kwa kidato cha tatu, kuna kopi moja kwa kila somo na kidato cha pili kuna kopi 10 kwa kila somo. Kuna kopi 13 kwa kila somo kwa kidato cha kwanza na uwiano katika shule hiyo ni mwalimu mmoja kwa wanafunzi 44.

Akizungumzia mitaala kwa shule za sekondari, anasema kwamba mabadiliko ya mara kwa mara ya mitaala ni tatizo kubwa kwa walimu na kwa ujumla mabadiliko hayo yanayumbisha sekta ya elimu nchini.

Anasema huwa hakuna taarifa wala maandalizi ya kufanya mabadiliko hayo na pia walimu hawashirikishwi.

No comments: