Wednesday, May 11, 2011

Mwingira Amtangazia Kifo Babu wa Loliondo


- Adai siku zake za kuishi zinahesabika

Kiongozi mkuu wa huduma ya Efatha, Mtume na Nabii Josephat Mwingira amemtangazia kifo Mchungaji mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Ambilikile Mwaisapila, maarufu kama Babu wa Loliondo, huku akisema siku za babu huyo kuishi sasa zinahesabika.

Akitoa tangazo hilo mbele ya waumini katika makao makuu ya huduma hiyo Mwenge, jijini Dar es salaam, Jumapili iliyopita, Mwingira alisema babu Mwasapila atakufa kwa kuwa amemtukana Mungu wa Mwingira kwa kuzidi kutamka kuwa tiba anayoitoa imetoka kwa Mungu.

Mwingira ametoa kauli hiyo ikiwa ni siku chache tu tangu atangaze rasmi vita dhidi ya Babu Mwasapila. Akitangaza vita  hiyo, Mwingira aliilaani tiba ya Babu huku akisema; “itoweke na iangamie kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti”

Katika tukio la Jumapili iliyopita, mwingira alisoma andiko kutoka Waebrania 1:1-2, kisha akasema Mungu haongei na miti huongea na wanadamu ambao ni watumishi wake. Aliendelea kusema kuwa, babu wa Loliondo amemkasirisha sana kwa kuwa amemtukana Mungu kwa kusema kwamba Mungu ameongea na miti na badala ya watumishi wake.

“Mungu haongei na miti, anaongea na watumishi wake, hata katika kuponya Mungu ameagiza tuweke mikono kwa wagonjwa, Marko 16:15-18 inafafanua hili. Sasa kwa sababu babu wa Loliondo amemtukana Mungu, naye siku zake zinahesabika, kwani Biblia inasema usimwache mchawi kuishi” alisema Mwingira.

Wakati akiendelea na mahubiri yake huku akipita kuombea wenye shida mbalimbali, ghafla alifuatwa na mtumishi mmoja wa kanisa hilo na kumweleza kuwa, ndani ya kanisa hilo amekamatwa msichana ambaye ametumwa kuloga ili kuharibu kazi ya Mungu.

Hata hivyo, Mwingira hakuonesha kushtushwa na taarifa hiyo badala yake aliendelea kuombea watu huku akisema; “mimi sitishwi na wachawi” baadaye wakati akiendelea kuombea watu waliofika eneo ambalo msichana huyo alikuwa ameanguka na kuamuru ainuliwe ili amhoji.

Miongoni mwa maswali aliyoulizwa msichana huyo ni wapi alikotokea na alikuwa ametumwa na nani. Katika majibu yake msichana huy0 alieleza kuwa ametokea Ngorongoro na ametumwa na mtu aliyedai amechoshwa na maombi ya Mwingira yanayokwamisha kazi zake za kichawi. Msichana huyo alitaja jina la aliyemtuma ambaye hatuwezi kuandika jina lake.

Msichana huyo alikutwa na pete yenye picha ya mtu aliyetajwa na msichana huyo kuwa ndiye kamtuma, pamoja na chuma kilichochongwa mfano wa fuvu lililobebwa na ndege pamoja na bangili kubwa ya shaba.

Baadaye Mwingira alimuuliza; “sasa nikufanye nini”? yule msichana akajibu; “naomba unisamehe sitarudia tena ufanya uchawi na sitarudi kule nilikotoka” Mwingira akamuuliza tena; “Unakubali kumpokea Yesu”? yeye akajibu; “ndiyo” Baadaye msichana huyo aliongozwa sala ya toba.

Mwingira ni mmoja wa viongozi wa dini ya kipentekoste ambao walikuwa wa kwanza kabisa kutangaza kuipinga tiba ya Babu wa Loliondo.

No comments: