Waziri Mkuu wa Misri, Essam
Sharaf, amevunja safari ya kuzuru nchi za Ghuba baada ya ghasia kati ya
Waislamu na Wakristo, zilizouwa watu kama sita.
Kwa kuvunja safari hiyo, Bwana Sharaf anaonesha anashughulishwa na ghasia nyengine zilizozuka baina ya makundi ya Waislamu na Wakristo.
Safari hii ghasia zimetokea kwenye mtaa wa kati-kati ya Cairo, pale kundi la Waislamu wa madhehebu ya Sunni, wanaoitwa Salafi, ambao hawapendi mabadiliko, lilipozingira kanisa ambamo likiamini Wakristo walikuwa wakimzuwia mwanamke, ambaye akitaka kubadilisha dini na kuwa Muislamu.
Risasi zilifyatuliwa, na kanisa na majengo mengine yalichomwa moto.
Ilichukua saa kadha kwa askari wa usalama kuzima mapigano.
Inafikiriwa kuwa Salafi ni wachache kati ya Waislamu, lakini wamekuwa na ghasia nyingi tangu Rais Hosni Mubarak kuondoka mwezi wa Februari.
Tangu wakati huo, kumetokea mapambano kadha baina ya Wakristo na Waislamu, na Wakristo wengi, ambao ni asili mia 10 ya watu wa Misri, wanahofia usalama wao, endapo makundi ya Waislamu wasiopenda mabadiliko, ndio yatashinda katika uchaguzi wa mwezi Septemba.
No comments:
Post a Comment